Lyrics



Nahodha

Wewe nahodha x2
shusha tanga pepo zime chachamaa!
Nanyi abiria pigeni mbizi,
muwezavyo chombo kimechota maji!
Haya wanafiki, vishuka,
nipeni leo hilo jina baya mniue!
Msoitakia mema nchi yangu,
nipeni leo hilo jina baya mniue!

Mlidhani wamelala mkateta mbele yao,
mkadhani ni watoto mkasema mbele yao!
Wamewasikia mkipanga mniue, eti mkate kauli, mzibe mdomo, ikibidi kwa kufuri, kama bado kiburi apewe nauli, arudi kwao Sumbawanga!

Walipowauliza nyie, bila haya mkajibu,
eti anatusema wala rushwa na sisi tumezoea,
anauponda ufisadi na huo ni mradi wetu eeh,
anatuvunjia heshima na sisi ni wanadini eeh,
Kwarezma tunafunga sie, Ramadhani tunafunga sie!
Anaingilia maisha ya watu,
hiyo sio tabia ya watanzania,
kwanza tuna mashaka na uraia wake eeh!
Na kuanzia leo ni marufuku radio yoyote kupiga nyimbo zake,
kiisaa anaimba ukweli eeh!

Wewe nahodha x2
shusha tanga pepo zime chachamaa!
Nanyi abiria pigeni mbizi,
muwezavyo chombo kimechota maji!
Haya wanafiki, vishuka,
nipeni leo hilo jina baya mniue!
Msoitakia mema nchi yangu,
nipeni leo hilo jina baya mniue!

Rushwa inakunyonya wewe mwananchi eeh!
Ufisadi unakubonda wewe mtanzania!
Nataka kukuokoa unanigeuka!
Wee jirani wewe, jirani yangu wewe!
Nyumba yako inachomwa, unapiga kelele,
“naona moto, naona moto” mi nnakuja kukusaidia,
unaona wanao wanateketea bila haya unaguna
eti “aah, kumbe taka za shimo tu zachomwa!”

Muheshimiwa rais naomba kijembe mi nikalimie mpunga,
nnashamba kubwa linafika darisalama!
Waheshimiwa wabunge nipeni vijembe vingi mi nikalimie mpunga,
nina shamba kubwa linafika Dodoma,
Maembe maembe mie, ng’ombe mwana yatima,
wacha nikimbie niponye wangu mtima,
ugali sinia zima waisha kwa yangu nyama,
ngozi yangu ndio njema kwa kuziwambia ngoma,
ikipigwa bagamoyo dunia nzima yavuma,
dunia nzima yavuma mama!
Rushwa imepewa heshima!
Ufisadi umesimama wima!
Nami siwezi nyamaza kimya!
Nchi inaangamia vijana tunaangalia!
Nchi inateketea wasomi tunachekelea!

Watu wa nchini kwangu eeh,
watanzania wenzangu tusijipake mavumbi,
mkole kuwa mwembeni sio kukosa ukumbi,
mijahazi imevunjika sembuse sie mitumbwi!
Itakuwa sie mitumbwi!

Wewe nahodha x2
shusha tanga pepo zime chachamaa!
Nanyi abiria pigeni mbizi,
muwezavyo chombo kimechota maji!
Haya wanafiki, vishuka,
nipeni leo hilo jina baya mniue!
Msoitakia mema nchi yangu,
nipeni leo hilo jina baya mniue!



Hamia Ndege

Labda ni mimi, labda si mimi,
labda nami nimo, labda mimi simo

Nalimwi anene, nalimwi ansanene x2

Hamia ndege, ooh hamia ndege,
hamia ndege, mwali wee hamia ndege,
hamia ndeegee,
mpunga wa baba, mpunga wa baba waliwa.
hamia ndeegee!

We kibaya na mpunga wangu eeh, umtima na ua langu eeh
Rushwa na maendeleo yangu eeeeh!

Hali inakuwa ngumu, hasa kwangu masikini,
pale nnapotakiwa nitie mkono mfukoni mwangu
ninunue haki yangu!
Mifuko imejaa miiba eeh, rushwa imebeba mimba wallah eeh!
Tuonyane vipi kwa mboni eeh? Nasi hatutazamani eeh!
Tukonyezane vipi nasi tupo gizani?

Makosa yote tenda mwanangu na lawama zije kwangu,
lakini hili la rushwa utalibeba peke yako!
Hili ni zito mwanangu, lahesabiwa mara tano kama dhambi ya wizi!
Yaani Kuiba, kutamani kuiba, kuweka mali ya wizi, kumficha mwizi,
na kumtamanisha mwizi ni dhambi ya wizi.
Nakuambia wewe mwanangu sababu wewe ni mdogo,
alafu nnakuweza!
Wakubwa siwawezi, wakubwa wana vishindo
 nami ni nyumba ya udongo tu, sihimiri kishindo!

Rushwa adui wa haki eeeeeeeeeeeeeeeeh!

Kipanga cheza ngoma, ntakupa mtoto wa kuku x2
Kipanga cheza ngoma, cheza ngoma, cheza ngoma,
ntakupa mtoto wa kuku,
Wanashangaza sana, eti toa chochote upate haki yako,
walimdanganya dada ati toa penzi ufauru mitihani,
wakamdanganya kaka ati toa chochote upate ajira yako

dada njoo tuwaimbe, kaka njoo tuwaimbe
wana mikono mipana – wanaomba rushwa
wana midomo mipana -  wanakula rushwa
wana matumbo mapana wameshiba rushwa
wana (matumbo mapana x3)

hamia ndege, mpuga wa baba mpunga wa baba waliwa
hamia ndege.



Kinoo

Fiicha kinoo chako,
koo la msema kweli,
lipo lipo hatarini,
lini litakwepa kisu?
Kisu kimesha nolewa,
leewa ubwabwaje ovyoo, lewa ubwabwaje ovyo.
Washanowa, noa wanapulula, washapulula pulula yote magamba, magamba magamba ya mti wangu eeh, ooh mti wangu eeh, mti wangu eeh, ooh nchi yangu eeh!

Kwanza mti si wangu, mti wa bibi kapanda uani kwangu! Na hata kama wa babu bado ni urithi wangu eeh!
Wamekuja tena ndugu zangu wa damu wameng’oa na shina wameondoka nalo eeh, walichuma majani, majani ya mti wangu eeh, wakafanya mboga mi nala ugalia mtupu eeh,
walikwarua magamba magamba ya mti wangu eeh, wamefanya dawa mimi nafa na magonjwa eeh,
wakachimba mizizi mizizi ya mti wangu wakaipika, mingine walikaanga, mingine wakaichoma wakafanya chakula mimi nakufa na njaa ee!
Ooh nchi yangu eeh, nchi yangu eeh, ooh nchi yangu eeh!

Nchi alirithi babu, babu akarithi baba, baba nikarithi mimi, mimi mnanipokonya warithi nini wanangu?
Nisemehe wapi eeh?
Ili mpate tambua kwamba mnaniumiza kuifuja nchi yangu eeh!
Urithi wa wanagu!
Nasemea mdomoni wanakosemea wenzangu ukweli hamuuoni eeh, ntasemea kwingine wasikosemea wenzangu mseme nimewatukana, mseme chafu lugha yangu eeh!
Some of our people, will have large amount of money, and spend on their life, while others have nothing!
Those who have received this prevelage must repay back sacrifice like others have made, they are like a man who have been given all food from a starving village, in order that he may bring back surplus from far distance.
If young men who have been given education by the people of this republic, and fail to use their knowledge for development of this country, they are traitors!
This is what I have been taught by Mwl. J Kambarage Nyerere, on may day 1964,
I aim to save my people with all I have got
I will always render services to people until the days comes for me to join my ancestors.

Ooh nchi yangu eeh, nchi yangu eeh, ooh nchi yangu eeh!



Toka

Toka eeeeeeh!
Toka eeh, iee, iee x2

Kulwa toka eee na Doto atoke x2
We mkubwa kwanini ukatalie mlangoni?
Hutaki kutoka eeh, hutaki kurudi ndani eeh,
Toka eeh, nasi tutoke,
Fanya toka wee mama apumzike!

Toka eeeeeeh!
Toka eeh, iee, iee x2

Tangu ndugu yetu alipozaliwa,
Siku zimepita miaka na miezi pia,
watu wanamwimbia,
eti kasimamaa peke yake,
anataka mdogo wake
Fanya toka wee mama apumzike!

Toka eeeeeeh!
Toka eeh, iee, iee x2

Toka eeh tukaseme kweli eeh,
Tumeambiwa tuitafute kweli,
Kwani kweli ndio itatuweka huru eeh,
Sisi eeh na dunia yetu eeh!

Mara nyingi kweli inaniweka shidani eeh,
Kweli ooh imeshaniponza mimi eeh
Ila sikomi kusema kweli,
Kweli ooh kwaajili yangu,
Kweli kwaajili ya nchi yangu,
Kweli kwaajili ya wanangu,
Oieeh na dunia yetu eeh.


Tuunakula sisi wanashiba wao eeh
Toka eeh tukaseme kweli eeh
Kazi sisi mishahara kwao eeh
Toka eeh tukaseme kweli eeh
Tulihenya sisi kiinua mgongo kwao eeh
Kwanini eeh tusiseme wazi eeh?

Tunasoma sisi wanafauru wao
Tumehitimu sisi shahada kwao
Tumefiwa sisi mirathi kwao
Wanakosa wao tunafungwa sisi eeh
Toka eeh tukaseme kweli eeh

Mambo mengine ya ajabu kweli eeh
Mengine yanatuchanganya
Wanaugua wao tunakufa sisi eeh!
Toka eeh tukaseme kweli eeh!


Hotuba

Wee mama nani weeh!
Mwagize mtoto aniletee mi ninywe nilewee, niongee kiingerezaa!
Mtume mtoto aniletee nije niuchape, niuchapee, nimwage ung’eng’ee!
Nikilewa situkani mimi huwa nalia, naimba au naongea kiingereza.

Ondoka ondoka wee katika nyumba yangu, nilipo kupata pesa za yule mgombea nikanywa nikalewa nikaanza kusema kinzungu “on taipu mai taipu isore wayawaya”
Nasi hatujambo, uchaguzi umeisha salama ila mwenzetu ndio analalamika eeh, kwamba mgombea alomuweka madarakani kwa kura yake mwenyewe, hamsaidii mamaa, hana maana kwake, haana mana!

Good morning house!
I give you comradely salute, “salaam”
I am the one who built you and put you where you are
I hope you know about this
I haven’t much time to spend here, but I would like to tell you something!
“Meetings come, Meetings  go
What shall I remember you for?
What have you done for the betterment of life?
Now and then I give you my good people
I also gave you power and I kept you in my home,
what haven’t you received from me house?
To whom much is given much is required!
You have given education and professionism to your youth,
 respect to the aged with experience, but the moment they get into your siting rooms they become weak

I expected to see the power of youth on these red chairs, wisdom of grey haired, magic of Beijing, but my expectation where not met!

Whom should I blame for this?
May be the one who advised me to decorate you with these luxuries!

I put a curse on the day I decided to build you, because you made my representatives to forget their Vows, they accuse God’s books they hold while swearing in, they accuse your day and time!
I am going to bomb you and no body will curse, then I will rebuild a new house and this family will stand again!
I set up a robust fort and I find a strategic position from which I can rain bombs, I rebuild by bombarding.

Wee mama nani weeh!
Mwagize mtoto aniletee mi ninywe nilewee,
niongee kiingerezaa!
Mtume mtoto aniletee nije niuchape, niuchapee,
nimwage ung’eng’ee!
Nikilewa situkani mimi huwa nalia,
naimba au naongea kiingereza.

Ondoka ondoka wee katika nyumba yangu,
nilipo kupata pesa za yule mgombea
nikanywa nikalewa nikaanza kusema kinzungu
“on taipu mai taipu isore wayawaya”
Nasi hatujambo, uchaguzi umeisha salama
ila mwenzetu ndio analalamika eeh,
mgombea alomuweka madarakani kwa kura yake mwenyewe,
hamsaidii mamaa, hana maana kwake, maana mana!






Barua 

Poooooh!
Pooza mtima eeh, mwaka huu tutavuna!
Pooza mtima, mwaka huu tutavuna, tuliza moyo mwaka huu tutavuna!

Natuma barua, majibu sipati x2
Natuma natuma, naambiwa haijafika mama eeh, nachoka ooh.

Gonga kingali moto, chuma gonga weeh!
Gonga kingali moto!

Nenda salama, safiri salama, kiunga chako cha minazi,
mintakilinda, wakija wezi wasilete madhara, nenda wee!
Nazi imara zimeshamiri angani, vidaka viso na afya vimeanguka,
mbata njema nimezihifadhi tutakula wote!
Kwa ujumla mambo si mabaya,
ila komba alitaka alete madhara,
alikwea mnazi afungue mitungi,
tembo tulogema wote ili anywe peke yake,
bahati njema mgema nilifunga ngangali nganganga,
kashindwa kufungua, kabaki analia,
“Mgema! Mgema!
Kwanini umefunga ngangali nganganga?
Hii ni mali ya umma!
Huoni aibu? Loooh, loooh”

Hata kama ni mali ya Umma ndio unywe peke yako?
Eti kisa ni mali ya Umma ndio ule peke yako!

Pooza mtima, mwaka huu tutavuna,
tuliza moyo mwaka huu tutavuna!



Majamvi

Waite waambie wajue x2
Majamvi nimetandika njee, na mengine baharini yanaelea!
Ni wale viongozi walojaliwa hekima ambao katika mtima imetambaa baridi wameacha watu wao, nchi zao na Afrikaa, tazama yanayo tufikaa.

Wazee mkienda mrudi eeh!
Basi mkienda muwe mnarudi nyieeh!

Mi natandika majamvi
Mi natandika nje!

Wakinyanyuka wazee niseme nao!
Akinyanyuka Nyerere niseme naye,
Akinyanyuka Karume niseme naye.

Mi natandika majamvi
Mi natandika nje!

Mmenyamaza nyie hamsemi,
mmenyamaza tena hamsemi eeh!
Fumbo mmeifumba midomo!
Sasa ooh nafungua zangu semi!
Ukimya umefikia kikomo!

Nishatandika majamvi nimetandika nje,
Na mengine baharini yanaelea.

Uhuru wetu unatukanishwa,
ukweli wa ukweli umebatilishwa!
Watoto wetu wamerithishwa,
tamaduni zisizo haki na heshima!
Hali ya maisha nayo ni ngumu,
vijana wenu walokosa uvumilivu
Utu wetu wanaunajisi
wanasema bora kuzaliwa mbwa utumwani
kuliko kuzaliwa watu nyumbani.
Mnawezaje kuyavumilia hayo,
nyinyi mnaojua dunia na kuzimu,
Mi natandika majamvi
Mi natandika nje!

Tumevuliwa akili ya elimu zetu,
tunatembezwa watupu hadharani,
mbele ya watoto na wakwe zetu,
nitawezaje kusema vingine?
Elimu niliyonayo inamaana gani,
cheti nimetundika ukutani,
akili yote ipo utumwani na hali ndugu zangu wapo shidani.
Nitawezaje kusema vingine,
nahali mimi nipo katika shida?
hatua chache tu tokea mauti,
mauti ya akili na ufahamu!
Ni heri nikatwe kichwa changu,
itanifaa nini mii kuishi nacho?
Kichwa hapa akili kule, kichwa cha leo akili ya majuzi ee
Mchuzi ee ushaingia kijusi.

Minsha tandika majamvi
Minsha tandika nje!

Mi natandika majamvi
Mi natandika nje!

Naanza na wewe Mwalimu,
wewe waijua historia ya nchi hii,
mbona babu zenu walisema nanyi
hata kabla hamjawaita, sisi ooh tumewakosea nini,
kulia msiba tu ama kuzika? Ama kuna lingine?
Nyie mafundi wa kuzika nyie udongo mlitupaje
hata wazee wagome kurudi?
Nakufuata hukohuko Butiama,
napita njia ya Manyara, kisha Ngorongoro,
kisha Serengeti, kisha nitokee pale Ikizu,
nipumzike kidogo kijijini Nyamswa,
kesho niteremkie bwawa la kyarano,
hapo nitaoga kidogo, jioni nipande juu Buturi,
kisha ooh niingie Butiama,
nifanye kikao nawe mwitongo, we mwalimu mpaka kieleweke….
Minshatandika majamvi nishatandika nje,
na mengine baharini yanaelea.
Wazee mkienda mrudi eeh!
Basi mkienda muwe mnarudi nyie!



Kwababa

Wako wengi eeh, wako wengi eeh x2
Wako wengi wanaonifanya mi niseme ooh
Wako wengi wanao nifanya mi nilie eeh!

Yako mengi eeh, yako mengi eeh
Yako mengi yanayonifanya mi niseme ooh
Yako mengi yanayonifanya mi niimbe eeh!

Nawahusia wana eeh, sia wana x2
Nawahusia wana kwa lugha ya Kiswahili
Kuna hili nahili ujuapo Kiswahili,
kuna taa na kandili ukijua Kiswahili,
hereni na bangili ujuapo Kiswahili,
kuna nyani na tumbili kasema Ahmad Nassir,
kuna bangi na bangili moja ikalie mbali eeh,
ukijua Kiswahili!

Nawahusia wana eeh, sia wana x2
Nawahusia wana kwa methali za Kiswahili eeh
Siku eeh ya mashaka fundo ooh
Tenda aah wema uende zako ooh,
kamwe ooh usingoje shukurani,
shukurani ya punda eeh huwa mateke eeh!
Tunasema waswahili eeh
Ashakum si matusi wanasema waswahili,
oh si matusi tunasema waswahili
yaani uniwie radhi kwa haya ninayosema
“mzigo wa mavi kamwe haubebeki hata ukibebeka
kamwe haupokeleki, ataupokea nani?
Niliwapa zangu tungo ziwafae maishani,
ooh zangu nyimbo ziwafae maishani
basi ndugu zangu walipokosa shukurani
wakakaa kikao wanitoe duniani,
kweli hawabebeki
isingelikuwa zangu tungo mi nisinge teseka,
kama si hizi nyimbo mi nisinge pata shida mama,
isingelikuwa za tungo mi wasinge nikamata
na kunitesa kama mbwa nakwambia
safari hii sitanyamaza, naapa na Mungu nita wasema kwa baba,
oh kwa baba naenda kusema kwa baba,
baaba ntasema kwa baba
mi nnaapa wallah mi nitasema kwa baba
na mchanga nnalamba naenda kusema kwa baba
walituma watu ee waje wanikamate,
wamenikuta mangesani mi napiga muziki ee
kwenye uzinduzi wa kempu ya masela
wameletwa pale na dugu yangu wa damu,
si mbangubangu ni mswahili mwenzangu
kipilipili mwenzangu mzaliwa wa hapahapa,
mi naapa na Mungu nitsema kwa baba.
oh kwa baba naenda kusema kwa baba,
baaba ntasema kwa baba
mi nnaapa wallah mi nitasema kwa baba
na mchanga nnalamba naenda kusema kwa baba



Hotuba ya mfungwa

Ndugu waheshimiwa na wote msioheshimiwa!

Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kuniweka hai na kunitia nguvu.
Hii ni hotuba ya kwanza kabisa ya mfungwa mswahili kwa watu wote, naiandika huku nikiomba mungu iwafikie ikiwa hivi nilivyoiandika, lakini sijui kama itawafikia wakati bado mwili wangu umeambatana na roho yangu.
Ndugu zangu, Jela inatuumiza!
Mimi ni mfungwa, kuwa mfungwa haimaanishi kuwa ni mtu mwovu bali ni mtu aliyeonwa na Sheria, Hapa nilipo ni mahala muhimu sana, ni mahala pakujenga. Ingawa wengi hutoka wakiwa wamebomoka na kuharibika kabisa, wamepoteza afya ya roho, akili na mwili.
Jela inawaumiza wanetu, Jela inawaumiza wazazi na wapenzi wetu ingawa hawapo kifungoni. Jela inaiumiza nchi yetu.

Ndugu zangu kuna umri wa kufundishana adabu lakini kwa nafasi hii niliyoipata wacha niitumie kwa kazi hii ingawa umri wenu umeenda!
Nafanya hivi makusudi kwa kujua kabisa kwani hata waswahili wamenionya kuwa samaki mkunje angali mbichi, akishakauka utamvunja bure upate lawama.
Ndugu Waheshimiwa, jiheshimuni, waheshimuni na wengine ili muheshimike kihalali!
Nanyi msioheshimiwa muwaheshimu wenzenu na mamlaka zilizowekwa, jiheshimuni pia ndipo mdai heshima.
Naomba nieleweke nimesema kuwa nimesema kuheshimu, sio kuogopa au kuabudu..

Nitaongea kwa mipaka ingawa leo nimepewa uhuru wa kuongea. Waswahili wamenionya kuwa Uhuru usio na mipaka ni utumwa. Haki ya nani Sijaona lugha tajiri kama hii.

Ndugu zangu!
Nilikuwa nasubiri kutolewa huku kwa msamaha wa rais nije kuongea nanyi ana kwa ana lakini bahati haijawa yangu labda mwakani.
Jamaa zangu chonde nawaomba mseme na roho zenu, Mungu ajaalie tuonane nyumbani tukiwa hai wote, tujenge taifa lililo jema.
Maisha ya jela ni magumu na ya hatari, lakini kuna wakati tunapata nafuu, hasa pale wanapoletwa wakubwa huku ndani, mlo unabadilika na dawa za mbu zinapulizwa, uji sukari kibao na maji safi kama kawaida, lakini tatizo hawakai sana… hata hivyo msemo wa Kiswahili huwa hauachi kutimia “mgeni njoo mwenyeji apone”. nduguzangu
kama nitajaaliwa kutoka  tutaonana nyumbani, ila sina matumaini sana maana wenye nguvu wameshaanza kunipiga kwa siri, kama roho yangu ikiachanishwa na mwili basi msisahau kuwaambia watoto wa leo kuwa Tanzania mpya ipo, Tanzania mpya bora ipo, ila wajikaze na waishike vizuri adabu yao.

Muheshimiwa mwongozaji!

Sikia sauti ya kilio cha mswahili tokea kwenye sakafu ya moyo wake.
Sikiliza bwana mkubwa, tutazame, nyuso zetu watanzania hazijui kudanganya, zinazungumza hali waziwazi tena kwa lugha nyepesi kabisa!
kuna kitu tumefanyiwa hapa!
Sijui ni kwa ubaya au kwa wema lakini ukweli ni huu.
Mmekamata vyombo vya habari, mmetukamata makoo, mnavipa ruhusa baadhi ya vyombo vya habari kuua maadili na utamaduni wetu! Mmeharibu mfumo wa elimu, alafu
Mnatutishia dini mnafikiri hatujui Mungu anataka nini?
Mnatutishia madaraka mnatufanya hatuijui Siasa safi ikoje?
Nakumbuka nilipokuwa shule ya vidudu sio chekechea, tulipofundishwa, mwalimu akiingia darasani monita anasema Heshma! Wote tunasimama na kusema,
“Ili tuendelee twahitaji vitu vinne, watu ardhi siasa safi na uongozi bora sisi vijana wa ccm tupo tayari kujenga taifa… shkaaaa mooo mwaalimu!” wakati huo ukisema nasema kweli tupu na chama kinilinde chama kinakulinda kweli. Kipindi hicho vtuo vya polisi haba mtuhumiwa akipatikana kwanza anafungiwa kwenye ofisi ya chama unasikia watu wanasema ‘kapelekwa zoni’
Ulaaniwe kujua, kujua si kwema, maana ningekuwa mjinga nisingepata shida akilini na moyoni kama hivi. Nimeishia darasa la nne tu nateseka hivi, je ninge….
Tofauti ipo! Tofauti kati ya Utawala bora na uongozi bora… tofauti ipo.

Tunategemea elimu ndio ituokoe lakini elimu yenyewe mitaala hailingani na maisha ya kweli! Kila kitu mnakitia siasa, mnakifanya biashara.
Utajiri wa nchi yetu ndio chanzo cha mateso kwetu. Hatufurahii maisha ndani ya nchi nzuri tuliyoachiwa na baba zetu.
Hivi, ni lini mtatupa fursa ya kuishi maisha yetu?
Ni lini tutafurahia uhuru wa nchi yetu? Tangu nchi inapata uhuru mpaka leo nchi inafikia nusu kalne, inahitaji uhuru mpya bado pua zetu hazijahisi hata kwa mbali harufu nzuri ya maendeleo.
Mnatuonesha kuwa njia rahisi ya mtu kuendelea ni kuwa mhalifu, sasa mnafikiri tutapungua huku jela?
Halafu nilitaka kusahau, niliona mambo yanaharibika nikaomba kusaidia mapambano dhidi ya rushwa nikaambiwa si kazi yangu, niliumia sana.

Halafu na wewe muweka kanda, nani kakupa kibari cha kazi hiyo wakati hujui unachofanya? Mnaona hii nchi ya kishkaaji sio? Hujakatazwa kupiga muziki wa waswahili redioni lakini nikikuletea ooh nisamehe kaka… maneno ya nyimbo zako hayatawafurahisha waheshimiwa… huu sio wakati wa kufurahishana huku nchi inaangamia, unaleta usomi wako wa kishamba bwana! Wamekuambia hawataki kusikia sauti ya kweli ya mswahili? Acha kujipendekeza wewe! Unajua kazi ya muziki wewe? Au unafikiri kazi ya muziki ni kujaza ukumbi wa disko na kuvutia watu kwenye kampeni? Ukome kujipendekeza, kama hujui hata wao waheshimiwa wana haki ya kuburudika, kujifunza na kusikia sauti za ukweli. Usiwanyime haki yao ya kupata taarifa, elimu na burudani.
Viongozi wangu wapendwa!
Mliniziba mdomo watanzania wenzangu wasinisikie kwakuwa siendani na matakwa yenu. Mkaweka uadui kati yangu na wenzangu.
Mkawapa nafasi wanamuziki wanafiki ili wawafichie uovu wenu, nyimbo za matusi zinaimbwa wazi wazi nanyi mnazichukulia poa tu.
Eti maendeleo, Chuo cha sanaa bagamoyo kinakufa mnajifanya hamuoni, chuo kikuu Dar es salaam kinazalisha matakataka mnachekacheka tu! subirini kidogo muone matokeo ya bomu mnalolitengeneza.
Mnaandaa mitaala ya elimu ya kuwajaza ujinga watu, mtu amehitimu lakini bado yuko uchi akilini.
Heri mimi sikusoma kabisa. Ila najua kuhesabu hela.
Wenye akucha makubwa wanatutesa, wanajificha nyuma ya siasa, biashara, na dini, watushambulia wanyonge bila huruma.
Alafu na nyinyi waumini mimi ndio nimewatoa maana kabisa kwa unafiki wenu! Na kwenye nyumba zenu za ibada mnifukuze kabisa mkitaka! Mungu atanipokea na kuwaaibisha wanafiki wakubwa nyie… mtu anasimama kashika katiba na kitabu cha Mungu wenu, anaapa kwa jina la Mungu alafu anaenda kinyume na kiapo chake kisha nyie mnamkenulia meno tu, mnajua maana ya kiapo nyie? Sawa katiba imepitwa na wakati, biblia na msaafu je? Mnashindwa kusimama kwaajili ya jina la Mwenyezi Mungu mtasimama kwaajili ya nani?
Nitasahau kusema yote lakini hili ntalisema kabla sijafa, Tanzania inataka katiba ya kitanzania, katiba ambayo si ya kikoloni, katiba ya zama hizi, ambayo hata tukiongozwa na bora kiongozi itamfanya aonekane ni kiongozi bora.
Katiba itakayo tuongoza kwenye maendeleo ya kweli, kumuheshimu Muumba aliyeamua kuusimamisha mlima Kilimanjaro tz, akaiweka ngorongoro na kutuzawadia bahari, akatupa ziwaTanganyika, nyasa, Rukwa, akajaza utajiri ardhini. Katiba itayoruhusu tume huru ya uchaguzi na pia taasisi huru ya kuzuia rushwa.

Nendeni mtoni mkaoshe akili na roho zenu ubinafsi umewachafua.. nasema mimi mfungwa mswahili, ashindikene! Mimi si yule msaliti anayesubiri nauli wakati aendapo ameshafika! Wala sina ujamaa naye, mie sitangazi ujomba ili nibebwe.
Msinichanganye kwanza nna mwiko wa kuchanganika na watu wanaoupenda sana uhai wao kuliko kuishi kwao.
Tofauti ipo! Tofauti kati ya Utawala bora na uongozi bora… tofauti ipo.

Siogopi maumivu mliyoniandalia, mimi ni marehemu niliyerudishwa kwaajili ya mswahili aliaye shidani? Mtu hafi mara mbili bwana.
Ndimi ashindikene bwana, kaulize bagamoyo, mimi pilipili, mimi dawa chungu, mimi nansimba, nene mwaromaini, nenu musilya nene nyimbwa zintaliwe, nene wakwe chomba chomba cha lushombo wakwe ntalenga nyama ulalenga na ya mulawa.
Nimetumwa naye mwenye uwezo wa kuumba na kuumbua anasema kwamba huu ndio wakati pekee ambao Sauti na na kalamu zetu zinaweza kuiokoa nchi  yetu kabla halijachwa jua la amani hii.
Ndugu wanafiki wafanyabiashara wa muziki, maadui wa utamaduni wetu wabinafsi na waabudu pesa wote!
Msijisumbue kunitishia umasikini, mkafikiri mtanibadilisha, mimi vita yangu sio ya utajiri na mali, sikuja na mizigo wala sihitaji mizigo katika kuondoka kwangu, nilikuja uchi kutoka tumboni mwa mamaangu nitarudi uchi katika tumbo la nchi.
Heshima ya nchi hii ya babaangu itarudi, kwa vyovyote na kwa gharama yoyote, kikiharibika kitu Babaanga atarekebisha, na sita kufa tena niwaache wanangu na njaa. mimi sio masikini na kila mtanzania aliyezaliwa baada yangu si mtoto wa masikini. Na njaa itamuheshimu, nene tundu kumusenga, wachisenga malezi nukumila ntaleka.
Tofauti ipo! Tofauti kati ya Utawala bora na uongozi bora… tofauti ipo.

Na wote mliotuibia
Imekuwa vema hatukufundishwa kushika siraha, na Muumba atunusuru na hilo, lakini ole wao watoto na wajukuu zenu, sijui wataoga wapi hata shombo na vumba la uozo wenu liishe, maana wanakuja watoto wetu hodari, wala nyuki, nyoka waumao usiku.
Mungu wangu, ulisha ibariki Tanzania Mungu ulishaibariki Afrika Mungu usituondelee Baraka hii. Sina haki saana ya kupewa kila nitakachoomba lakini kwa neema zako naamini utanijaalia kwaajili ya Tanzania yako.
Tofauti ipo! Tofauti kati ya Baraka na laana… tofauti ipo. Watie haibu maadui
wa mtumishi wako - Amlaanie uliyembariki laana yake imrudie.